Na Lucas Mboje, Dar es Salaam
WATUMISHI
wa Jeshi la Magereza wametakiwa kuzingatia utendaji kazi wenye tija
mahala pa kazi na kuacha kufanya kazi kwa mazoea(Business as usual).
Rai
hiyo imetolewa na Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, John Casmir
Minja wakati akizungumza kwenye Baraza la kufunga Mwaka 2015 na
kuukaribisha Mwaka mpya 2016 katika Ofisi za Makao Makuu ya Jeshi hilo
Jijini, Dar es Salaam.
Jenerali Minja amewaagiza Watumishi wote
wa Jeshi hilo kuhakikisha kuwa wanawajibika kwenye maeneo yao ya kazi
ili kufikia ufanisi uliotarajiwa pamoja na kutumia vizuri rasilimali za
Ofisi kwa manufaa yaliyokusudiwa.
"Utekelezaji wenu wa kazi za
kila siku lazima uwe na tija na uendane sambamba na kasi ya Serikali ya
Awamu ya Tano ili kufikia ufanisi unaotarajiwa". Alisema Jenerali Minja.
Aidha
Jenerali Minja amezungumzia baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kwa
Mwaka 2015 ambayo ni pamoja na kukamilika kwa Sera ya Taifa ya Magereza
ambayo italiwezesha Jeshi hilo kutekeleza mpango wake wa Maboresho ya
maeneo mbalimbali, kusainiwa kwa Mkataba na Kampuni ya Poly Teknology
ya China itakayojenga nyumba 9,500 za Makazi ya Maafisa na Askari,
kusainiwa kwa Mkataba wa Magari 9,05 na Kampuni ya Ashok Leyland ambapo
magari hayo yanatarajiwa kupokelea mapema mwakani.
Mafanikio
mengine ni pamoja na Usajili wa kudumu wa Chuo cha Urekebishaji ambapo
Chuo hicho kitatoa elimu stahiki ya Urekebishaji itakayotambulika ndani
na nje ya Nchi, Jeshi la Magereza limepeleka Maafisa wake kwenye
shughuli za Ulinzi wa Amani kwenye nchi mbalimbali zenye migogoro, Jeshi
limeingia ubia na Wawekezaji mbalimbali katika miradi ya Kilimo,
uchimbaji madini ya chokaa, ujenzi wa maduka makubwa(shopping Malls)
katika Mikoa ya Morogoro na Kilimanjaro ambapo miradi hiyo itakuwa na
manufaa makubwa kwa Jeshi.
Vilevile Jeshi limefanikiwa kuandaa
Maandiko mbalimbali ikiwemo andiko la kujitosheleza kwa chakula na
miradi minane ambayo miradi hiyo ikiwezeshwa inaweza kuongeza thamani za
mali zinazozalishwa na Jeshi hilo.
Aidha Jenerali Minja alieleza
changamoto mbalimbali ambazo Jeshi hilo linakabilianazo ambazo ni
ufinyu wa bajeti, uhaba na uchakavu wa vyombo vya usafiri, ukosefu wa
zana za kilimo, mabadiliko ya hali ya hewa hivyo kuathiri Uzalishaji,
tatizo la miundombinu ya magereza na msongamano magerezani hali
inayopelekea kwa kiasi fulani kuathiri utekelezaji wa majukumu ya Jeshi
hilo.
Kamishna Jenerali wa Magereza, John Minja ametoa Salaam za
kheri ya Mwaka mpya 2016 kwa Watumishi wote wa Jeshi hilo na kuwataka
kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zinazotawala
uendeshaji wa Jeshi la Magereza.
(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza)