Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Philip Isidor Mpango, leo tarehe 24 Oktoba, 2024 amefungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza ambapo Mkutano huo wa siku mbili unalenga kufanya tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya Jeshi la Magereza na kuweka mikakati ya kuboresha utendaji kazi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo Dkt. Mpango amesema, Jeshi la Magereza lishirikiane na Jeshi la Polisi pamoja na Bodi ya Taifa ya Parole ili kuweka utaratibu wa pamoja wa kuwatambua na kuwafuatilia wale wote wanaotoka Magerezani baada ya kumaliza vifungo vyao ili wawezeshwe kwa kupewa mikopo kutoka kwa Halmashauri zinazowazunguka itakayowasaidia kufanya biashara na kujikimu kimaisha ili kuwaepusha kurudi tena Magerezani.
Dkt. Mpango pia amesema, mchakato wa marekebisho ya Sheria ya Magereza ni mchakato muhimu lakini hautakua na maana iwapo Maafisa na askari hawatabadilika kimtazamo kuendana na mazingira, kwa kuwa Sheria na mifumo ya Magereza tuliyo nayo tumeirithi kutoka kwa wakoloni hivyo ameitaka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuharakisha marekebisho ya Sheria hiyo yanafanyika haraka na yazingatie mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai.
Makamu wa Rais aliendelea kusisitiza kuwa mkutano huu usaidie kuleta mitazamo chanya ndani ya Jeshi la Magereza kuhusu mabadiliko na kujitosheleza kwa chakula ikiwa ni pamoja na kuzalisha miche na mbegu bora za mazao tofauti ya kimkakati ili kuondokana na utegemezi kutoka nje ya Nchi huku akisisitiza kuwa Viwanda vyetu vya ndani na vile vya ubia vinazalisha na kukidhi masoko ya ndani ya Nchi.
“Ili kuendelea kuboresha kilimo na kujitosheleza kwa chakula Jeshi halina budi kununua au kukopa zana bora za kilimo kutoka taasisi binafsi ili kuzalisha chakula kwa aajili ya Wafungwa na Mahabusu” Alisema Dkt. Mpango.
Aidha Dkt. Mpango amelitaka Jeshi la Magereza lishirikiane na Wakala wa Misitu Tanzania ili kuweza kuzalisha miche ya miti na matunda ili liwe kielelezo cha utunzaji wa Mazingira.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh. Mhandisi Hamad Masauni amesema,ndoto ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuona Jeshi la Magereza linatumia rasilimali zake kikamilifu ikiwemo ardhi ili kuzalisha kwa tija na kujitosheleza kwa chakula na kutoa mchango kwa Taifa ili kutatua changamoto ndani ya Jeshi na kuipunguzia mzigo Serikali.
Naye Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP) Jeremiah Yoram Katungu amesema, mwelekeo wa Jeshi la Magereza ni kuhakikisha tunaboresha Programu za Urekebishaji wa Wafungwa ili ziendane na wakati uliopo na kwa kuzingatia Sheria za nchi, Kikanda na Kimataifa.
Aidha CGP. Katungu ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi inavyoliwezesha Jeshi la Magereza kutekeleza majukumu yake kwa kuliongezea bajeti, kuajiri askari wapya na kuwapandisha vyeo maafisa na askari katika ngazi mbalimbali wapatao 11,880 kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2020/2021 hadi mwaka 2023/2024.
Hafla ya ufunguzi wa mkutano wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza imehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali.