Banner

Banner

Friday, October 4, 2024

KATIBU MKUU WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI AFANYA ZIARA MAGEREZA MAKAO MAKUU, AZINDUA MAGARI MAPYA 11

 Na. Sgt. Geofrey Jacka - DODOMA


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ndg. Ally Senga Gugu, akikata utepe kuashiria Uzinduzi wa Magari 11 ya Jeshi la Magereza.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ndg. Ally Senga Gugu, leo Oktoba 02, 2024 ametembelea Makao Makuu ya Jeshi la Magereza eneo la Msalato Jijini Dodoma na  kupokelewa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Jeremiah Y Katungu, pamoja na maafisa wa ngazi mbalimbali.


Akizungumza na Maafisa, Askari na Watumishi wasio Askari Katibu Mkuu Gugu amesema, lengo la ziara hiyo ni kujitambulisha ili kufahamiana na kupeana Miongozo ya kiutendaji wa kazi huku akiahidi Ushirikiano na Viongozi wa Jeshi la Magereza katika kutatua changamoto zinazowakabili watumishi na kusisitiza umoja na ushirikiano miongoni mwa watendaji. 


Aidha Ndg. Gugu ameutaka Uongozi wa Jeshi la Magereza kutumia falsa ya 4R ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inabeba  Ujumbe wa Maridhiano (Reconcilation)  Ustahamiliivu (Resilience) Mabadiliko (Reforms) na Kujenga Upya yaani Rebuilding, ambayo imeonesha mafanikio  makubwa pale inapotekelezwa kikamilifu.


Kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu kuzungumza, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP) Jeremiah Katungu alitoa maelezo ya kina kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na Jeshi la Magereza nchini na kumshukuru Katibu Mkuu Kwa kutenga muda wake kufanya ziara ndani ya Jeshi la Magereza.


Katibu Mkuu Ndg. Ally Senga Gugu pia alipata fursa ya kuzindua Magari 11 ya Jeshi la Magereza yatakayo tumika katika shughuli za kiutawala, pamoja na gari moja la kubebea wagonjwa (Ambulance ) ambalo litapelekwa Hospitali Kuu ya Jeshi la Magereza iliyopo Ukonga, Jijini Dar es Salaam.