Banner

Banner

Friday, July 11, 2025

CGP. JEREMIAH KATUNGU AWAVISHA VYEO VIPYA MAAFISA 839 WA JESHI LA MAGEREZA

Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini CGP Jeremiah Yoram Katungu,leo Julai 11, 2025 amewavisha vyeo vipya maafisa 29 wa Magereza Makao Makuu,  ikiwa ni miongoni mwa maafisa 839 waliopandishwa vyeo kwa kada mbalimbali katika Jeshi la Magereza Tanzania  bara, kwa mwaka 2024/2025.

Akizungumza katika hafla hiyo ya uvalishaji vyeo CGP. Katungu  amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwa kuliwezesha Jeshi la Magereza kutekeleza majukumu yake na kutoa kibali cha upandishaji vyeo  kwa Maafisa hao. 

Aidha, CGP. Katungu amewapongeza maafisa wote walio panda vyeo nchi nzima na kuwataka kufanya kazi kwa uweledi,uadilifu huku akieleza kuwa ni matarajio ya Jeshi na Serikali kwaujumla kuwa watatekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa na kutanguliza mbele maslahi na ustawi wa Jeshi la Magereza na Taifa kwaujumla.

Kwaupande wake Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza CP. Nicodemus Tenga, amewapongeza Maafisa wote waliopandishwa vyeo na kuwataka wakatafute suluhisho la matatizo yaliyopo katika sehemu zao za kazi ili kuleta ufanisi wakiutendaji katika Jeshi.

Akitoa neno la shukrani kwaniaba ya wote waliopandishwa vyeo, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Elmas Mgimwa, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuridhia kibali cha upandishaji vyeo pamoja na Tume ya Utumishi wa Jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto na Uokoaji na Uhamiaji na uongozi mzima wa Jeshi la Magereza kwa kuwapendekeza.

Maafisa hao wamepandishwa vyeo kuanzia Julai 07, 2025 kwa mujibu wa Muundo wa Maendeleo ya Utumishi wa Jeshi la Magereza wa mwaka 2015 na kuzingatia Ikama ya Jeshi.

Wednesday, April 16, 2025

WAKUU WA MAGEREZA MIKOA NA MAGEREZA YOTE NCHINI WAPONGEZWA UTEKELEZAJI MATUMIZI YA NISHATI SAFI


Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini (CGP) Jeremiah Yoram Katungu amewapongeza wakuu wa Magereza mikoa na Magereza yote nchini kwa utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.


Pongezi hizo amezitoa Aprili 15, 2025 kwenye kikao kazi kilichofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Jeshi la Magereza Msalato jijini Dodoma.


"Ninayo furaha Magereza yote nchini tumeachana na matunizi ya kuni na sasa tunatumia nishati safi ya kupikia" Alisema CGP Katungu.


Pia, CGP. Katungu amewataka kutorudi nyuma katika matumizi ya kuni, badala yake waendelee kutumia nishati safi ya kupikia kama Serikali ilivyoagiza.


Aidha, CGP. Katungu, amewaeleza Wakuu wa Magereza mikoa na Magereza kuwa Jeshi la Magereza limefanya ushirikiano na taasisi ya Elimu na Mafunzo ya ufundi stadi (VETA) na hivi karibuni imeweza kutunuku vyeti wafungwa 201.


Vilevile, Jeshi la Magereza linaendelea na mazungumzo na Chuo cha Uhasibu Arusha ili kuanza kutoa masomo kwa njia ya mtandao(online) kwa kuanzia na masomo ya ujasiliamali kwa wafungwa magerezani.


Pia, CGP Katungu amewataka watumishi wote wa Jeshi la Magereza kudumisha upendo, mshikamano miongoni mwao kwaajili ya maendeleo ya Taifa.


Kwa upande wake,Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, (CP)Nicodemus Tenga 

amewataka wakuu hao wa Magereza mikoa na Magereza yote nchini kukusanya taarifa za wafungwa wenye sifa zitakazowezesha kujadiliwa katika Bodi za Parole kwa kuwa mchakato wa kumjadili mfungwa huanzia katika Kamati za urekebishaji ya Gereza, ili wafungwa wenye sifa ya kunufaika na mpango huo wanatakiwa wapatiwe.


Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Wakuu wa Magereza mikoa na Magereza yote nchini, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mwanza Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Masud Kimolo, alimshukuru Mkuu wa Jeshi la Magereza (CGP) Jeremiah Katungu nakuahidi maelekezo yote ambayo ameyatoa watayatekeleza na kufanya kazi kwa weledi wa hali ya juu kwa manufaa ya Jeshi na Taifa kwa ujumla.

Saturday, March 29, 2025

WAHITIMU WA KOZI YA UONGOZI WA JESHI LA MAGEREZA WATAKIWA KUONESHA WELEDI KAZINI


Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati, Mhe. Dotto Biteko (Mb), ametoa Wito kwa  Wahitimu wa Kozi ya Uongozi wa Ngazi ya Juu (GO'S) Jeshi la Magereza, kutumia maarifa waliyopata kuboresha utendaji kazi, kudumisha nidhamu, sambamba na kuleta magaeuzi chanya ndani ya jeshi.

Mhe. Biteko amezungumza hayo katika hafla ya kufunga Kozi namba 27 ya Uongozi wa juu iliyofanyika katika viwanja vya Chuo Cha Taaluma ya Sayansi ya Urekebishaji Tanzania (TCTA) jijini Dar es Salaam, Machi 28, 2025 ambapo aliwapongeza wahitimu kwa hatua waliyoifikia na kuwakumbusha kuwa kupandishwa cheo ni ishara ya kuongezewa majukumu makubwa zaidi.

"Serikali inatarajia kuona mnakuwa chachu ya mabadiliko katika Jeshi la Magereza kwa kufanya kazi kwa bidii, uadilifu, na kuhakikisha haki inatendeka kwa mujibu wa Sheria," alisema Mhe. Biteko.

Naibu Waziri Mkuu, Alisisitiza kuwa Jeshi la Magereza lina jukumu kubwa la kuwahudumia watu waliokosea, lakini lengo kuu ni kuwasaidia kurekebisha tabia zao ili wawe raia wema wanaporejea kwenye jamii. Aliwataka wahitimu kuhakikisha wanazingatia utu, weledi na kuzingatia Sheria, taratibu na kanuni za kazi.

Kwa Upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo amesisitiza dhamira ya Serikali ya kuleta mageuzi katika Taasisi za Haki Jinai kama sehemu ya juhudi za kuboresha mifumo ya utoaji haki nchini.

Aliongeza kuwa hatua hiyo inatokana na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye aliunda Tume Maalum ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai ili kutathmini changamoto zilizopo na kupendekeza njia bora za kuimarisha Sekta hiyo.

Naye, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP) Jeremiah Katungu, amesema kuwa, Jeshi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) lilizindua mpango wa kurasimisha ujuzi wa wafungwa, ambapo jumla ya wafungwa 201 wamepatiwa vyeti rasmi. Lengo la mpango huo ni kuhakikisha ujuzi walioupata Magerezani unatambulika rasmi ili kuwawezesha kupata ajira au kujiajiri mara baada ya kumaliza vifungo vyao.

Tuesday, March 18, 2025

KAMATI YA BUNGE YA AFYA NA MASUALA YA UKIMWI YAFANYA UKAGUZI ZAHANATI YA GEREZA SINGIDA.

 

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi, ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Hassan Mtenga, imefanya ziara ya ukaguzi katika  Zahanati ya Gereza Singida, leo machi 17, 2025, ikiwa na lengo la kutathmini huduma zinazotolewa zahanati hapo.

 

Katika ukaguzi huo  Kamati ilikagua huduma za CTC, chumba  cha Maabara, chumba cha daktari, chumba cha takwimu pamoja na chumba cha  dawa,  pia  waliweza kufanya  kikao na Kamati ya mkoa ya Afya  na masuala  ya  Lishe  na kuupongeza uongozi wa  jeshi la magereza kwa huduma  wanazotoa katika zahanati hiyo.


"Hongereni kwa kazi kubwa na nzuri ambayo  mnafanya, tumejionea ,  DMO pamoja na  dactari mkuu wa mkoa  tunaomba  mtatue changamoto ndogondogo zinazokabili  zahanati ya gereza" alisema  Mhe. Mtenga


Aidha Mhe. Mtenga ametoa rai kwa Wajumbe wa Kamati hiyo pamoja na wabunge wote nchini  kujenga utamaduni wa kutembelea  Magereza mbalimbali ili kubaini changamoto zinazoyakabili na kuzitafutia ufumbuzi.


Kwaupande wake Kamishina Jenerali wa  Magereza  Jeremia  Yoram Katungu  ameishukuru  Kamati ya Bunge  ya Afya na Masuala ya  Ukimwi kwa kutembelea na kukagua Zahanati hiyo na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote waliyoyatoa ili kuboresha huduma za Afya

Monday, March 17, 2025

KAMATI YA BUNGE MAMBO YA NJE ULINZI NA USALAMA (NUU) YATEMBELEA GEREZA KUU ISANGA.


Kamati ya Bunge Mambo ya Nje Ulinzi na Usalama (NUU) ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Vita Kawawa, Machi 13,2025,  wametembelea Gereza Kuu Isanga jijini Dodoma kujionea miradi mbalimbali inayoendelea katika Gereza hilo pamoja na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Gereza Maalum.


Akizungumza mara baada ya ukaguzi ujenzi wa Gereza Maalum, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Vita Rashid Kawawa ameonesha kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi na kulipongeza Jeshi la Magereza kwa kusimamia kikamilifu Fedha za Serikali katika kutekeleza mradi.


‎Aidha Kamati hiyo imelipongeza Jeshi la Magereza kwa kutekeleza agizo la Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia vema matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiwemo matumizi ya mkaa mbadala(Briquettes),Gas asili(Natural Gas) magerezani na kufanikisha kuondokana na nishati chafu. 

‎Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP) Jeremiah Katungu ameishukuru kamati hiyo kwa mafanikio aliyoyapata kwa bajeti ya mwaka 2023/24 na kufanikisha ukarabati wa Gereza maalum liliopo eneo la Gereza kuu Isanga.

‎"Jeshi linaishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama kwa namna anavyoliwezesha Jeshi la Magereza katika kutekeleza majukumu yake ya msingi ikiwemo miradi ya kimaendeleo" alisema CGP. Jeremiah Katungu.

ZIARA YA NDC MAKAO MAKUU YA MAGEREZA


Wakufunzi na wanafunzi kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC),leo Machi 12,2025 wamefanya ziara Makao Makuu ya Jeshi la Magereza Msalato jijini Dodoma, lengo likiwa ni kujifunza shughuli mbalimbali zinazofanywa na Jeshi la Magereza.

Akiongea katika hotuba yake Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP)Jeremiah Yoram Katungu amekipongeza Chuo hicho kwa kufanya ziara Makao Makuu ya Jeshi la Magereza huku akisema uhusiano huo unalenga kujenga na kuimarisha katika muktadha wa kulinda mataifa yetu kuendelea.

Kwa upande wake Brigedia Jenerali C.J.Ndiege ambaye ni mkuu wa msafara kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) amesema kuwa miongoni mwa malengo ya Chuo hicho ni kutoa mafunzo ya kimkakati katika masuala ya ulinzi kwa sekta binafsi, kikanda na kimataifa.

Aidha katika ziara hiyo kulitolewa wasilisho la matumizi ya teknologia ya habari magerezani,ambapo wasilisho hilo lilitolewa na Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Kizito Jaka.


Pamoja na mambo mengine washikiri katika ziara hiyo walipata fursa ya kupanda miti eneo linalozunguka Makao Makuu ya Jeshi la Magereza.

WAZIRI BASHUNGWA ATUNUKU VYETI KWA WAFUNGWA 201 WALIOHITIMU MAFUNZO GEREZANI

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Innocent Lugha Bashungwa (Mb), leo Machi 11, 2025 amezindua Programu ya Urasimishaji wa ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa mafunzo (Recognition of Prior Learning - RPL) na kuwatunuku vyeti vinavyo tambulika na VETA Wafungwa 201 waliohitimu Mafunzo ya fani mbalimbali yaliyotolewa na Jeshi la Magereza.


Akizungumza katika hafla hiyo ya utoaji vyeti Mhe. Bashungwa alisema Programu hiyo itatoa hamasa kwa wafungwa kujifunza na kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za urekebishaji ili kupata ujuzi, elimu, na maarifa kwa ajili ya kuwasaidia kujiajiri au kuajiriwa pindi watakaporudi katika jamii baada ya kutumikia vifungo vyao magerezani. 


Kwaupande wake Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP) Jeremiah Yoram Katungu, ameishukuru Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi stadi (VETA) kwa kukubali kuingia makubaliano na Jeshi la Magereza na kutoa vyeti kwa Wafungwa wanohitimu fani mbalimbali Magerezani.


Hafla ya utoaji vyeti kwa Wafungwa ilifanyika Chuo KPF Mkoani Morogoro ambapo Wafungwa waliotunukiwa vyeti wamehitimu katika fani ya Umeme, Ujenzi, ufundi rangi, bomba, magari, upishi, ushonaji na Seremala.

Thursday, February 27, 2025

WAFUNGWA 118 KUNUFAIKA NA MPANGO WA PAROLE


Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole  Mhe. Balozi Khamis Kagasheki Feberuari 20, 2025 aliongoza kikao cha 52 cha  Bodi ya Taifa ya Parole kilichofanyika kwa muda wa siku mbili katika Ukumbi wa Corridor Springs Hotel jijini Arusha ambapo 
wajumbe wamejadili na kupendekeza wafungwa ambao wana sifa ya kunufaika na mpango wa Sheria ya Parole.

Pia Mhe. Kagasheki alisema kuwa wafungwa waliojadiliwa wameshatumikia sehemu ya kifungo chao gerezani na kifungo kilichobaki wataenda kumalizia wakiwa na familia zao na jamii kama Sheria ya Parole inavyotaka.

''Bodi imepitia kwa umakini majalada 132 na kuona kama vigezo, Kanuni, taratibu na Sheria zimefuatwa  hivyo basi Bodi imeamua kuwa wafungwa 118 wanastahili kunufaika na mpango huo wa Parole'' Alisema Kagasheki.

Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini (CGP) Jeremiah Yoram Katungu ametoa rai kwa jamii na wananchi kwa ujumla kushirikiana kwa pamoja na Jeshi la Magereza kuwapokea Wafungwa ambao wanatarajia kutoka gerezani kwa mpango wa Parole, nakusema kuwa Wafungwa hawa wamejirekebisha kitabia na mienendo yao wakiwa gerezani.

Pamoja na mambo mengine CGP Katungu alisema kuwa utaratibu wa Parole umewekwa kwa mujibu wa Sheria na umeainisha vigezo ambavyo vinatakiwa kuzingatiwa ili mfungwa aweze kunufaika na mpango huo, akivitaja vigezo hivyo ikiwemo urefu wa kifungo chake, tabia na mwenendo wake akiwa gerezani, lakini kama jamii nayo iko tayari kumpokea, hayo yote yanazingatiwa wakati Bodi inamjadili mfungwa huyo ili aweze kupendekezwa kwa utaratibu wa Parole.

Kikao hicho cha 52 cha Bodi ya Taifa ya Parole kimejadili jumla ya majalada 132, na majalada 118 yamekidhi vigezo vya mpango huo.

WAZIRI BASHUNGWA AZINDUA MABASI YA KUSAFIRISHA MAHABUSU KWENDA NA KURUDI MAHAKAMANI

 


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Innocent Lugha Bashungwa, Februari 14, 2025 alifanya ziara Makao Makuu ya Jeshi la Magereza na kuzindua Mabasi Saba ya kubebea Mahabusu kwenda na kurudi Mahakamani.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mabasi hayo Mhe. Bashungwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri na kubwa anayo endelea kuifanya ya kuboresha Jeshi la Magere

za kwa kulipatia vifaa na vitendea kazi mbalimbali ikiwemo mabasi tuliyo yazindua na kutoa wito wa kuyatunza magari hayo ili yadumu na kutoa huduma iliyokusudiwa.

"Nitumie nafasi hii kumshukuru sana Rais wetu na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambayo anaendelea kuifanya yakuboresha Jeshi letu la Magereza, kuliwezesha Jeshi letu la Magereza kuwa na vifaa na vitendea kazi kama ambavyo tumeshuhudia uzinduzi wa mabasi haya ambayo yanaenda kuboresha huduma kwa ndugu zetu wafungwa" alisema Mhe. Bashungwa

Aidha,  Mhe. Bashungwa amelipongeza Jeshi la Magereza nchini kwa kutekeleza kikamilifu jukumu la kuwapa ujuzi wafungwa ikiwemo ufundi stadi na kuuendeleza ujuzi wa wafungwa wanaoingia nao, huku akieleza mkakati uliopo wa kuzindua program maalum kwa kushirikiana na VETA ili kutoa vyeti kwa wafungwa baada ya kupata ujuzi Gerezani.

Katika hatua nyingine Mhe. Bashungwa amempongeza CGP. Katungu kwa kusimamia agizo la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, la kuachana na matumizi ya kuni na kuanza kutumia nishati safi ya kupikia katika Magereza yote hapa nchini.

Monday, November 25, 2024

CGP. KATUNGU AFANYA KIKAO NA WAKUU WA MAGEREZA YOTE TANZANIA BARA

Mkuu wa Jeshi la Magereza Nchini (CGP  Yoram Katungu Novemba 23, 2024 alifanya kikao kazi na wakuu wa Magereza  Mikoa yote Tanzania bara na kuwataka wakuu hao kutokuwa na makundi, mivutano na migongano mahala pa kazi na kuhimiza Umoja, Ushirikiano na Upendo ili kuwa na mwelekeo mmoja kama Jeshi.


CGP. Katungu, alisisitiza masuala mbalimbali ya kiutendaji ikiwemo programu za mfungwa anapoingia gerezani afanyiwe tathmini ya kina ili kugundua uwezo wake na kumpangia program ya  kumfaa katika kufanikisha suala la Urekebishaji kwa mfungwa husika na pindi anapokaribia kumaliza kifungo chake, aandaliwe kisaikolojia namna bora ya kwenda kuishi na jamii ukizingatia kwasasa Jeshi linafanya  mapitio ya Sheria ya kuwafuatilia wafungwa pindi wanapokuwa wamemaliza vifungo vyao.

Kwa upande wake Mkuu wa Divisheni ya Fedha na Mipango Kaimu Kamishna wa Magereza (DCP) Chacha Bina, alipongeza wakuu wa Magereza kwa jitihada zao za kuhakikisha maduhuli ya serikali yanapatikana kwa wakati na kuvuka malengo ya kukusanya maduhuli hayo akisisitiza kuwa maduhuli si takwa la Mkuu wa Jeshi, bali ni agizo la Serikali.


Katika kikao kazi hicho wakuu wa Divisheni, Vitengo na Sehemu waliwasilisha mada mbalimbali.



Thursday, November 7, 2024

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA ARIDHISHWA MIUNDOMBINU YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA GEREZA ISANGA.

 Na. Sgt. Geofrey Jacka - DODOMA


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa (Mb), leo Novemba 07, 2024 amefanya ziara ya kikazi Gereza Kuu Isanga jijini Dodoma, kwa lengo la kukagua maendeleo ya utekelezaji wa agizo la Serikali kuhusu Matumizi ya Nishati safi ya kupikia Magerezani, ambapo ameeleza kuridhishwa na utekelezaji unaondelea Gerezani hapo.

Akizungumza mara baada ya kukagua Miundombinu hiyo Mhe. Majaliwa amesema, Serikali imeunda Kamati ya Kitaifa ya kusimamia kampeni ya Matumizi ya Nishati safi ya kupikia inayojumuisha Tanzania Bara na Zanzibar na umewekwa mpango kazi wa namna ya kuendesha kampeni huku kukiwa na Mkakati wa miaka kumi kuanzia 2023 hadi 2033 kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wote wanatumia Nishati safi ya kupikia.

"Niwapongeze sana Jeshi la Magereza kwa kuanza kutumia Nishati safi ya kupikia Magerezani, kwani Serikali tumeshaunda Kamati ya kusimamia kampeni ya Matumizi ya Nishati safi na Mpango kazi wa namna ya kuendesha kampeni hiyo ili kufikia 2033 asilimia 80 ya Watanzania wote  wawe wameachana na Matumizi ya kuni na kutumia nishati safi ya kupikia, hivyo niwapongeze sana Magereza kwa kuanza teknolojia hii". Alisema Mhe. Majaliwa 


Aidha Mhe. Majaliwa amemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mhandisi Hamad Masauni, kuhakikisha anasimamia kikamilifu zoezi la matumizi ya Nishati safi ya kupikia kwa Magereza yote Nchini na kutoa taarifa ya ukamilishaji ifikapo  Desemba Mwaka huu 2024, huku akieleza kuendelea na zoezi la Ukaguzi wa mara kwa mara kuhakikisha Taasisi zote zinatumia Nishati safi ya kupikia.


Kwaupande wake Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mhandisi Hamad Masauni amesema anaishukuru Serikali kufuatia ongezeko la bajeti ya Wizara kutoka wastani wa Shilingi Milioni 936 hadi kufikia Trilioni 1.7 ambayo inagusa maeneo mengi ikiwemo kuboresha Miundombinu ya Magereza.


Akitoa ripoti ya utekelezaji wa Mpango wa Matumizi ya Nishati safi ya kupikia Magerezani, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP) Jeremiah Yoram Katungu amesema, Jeshi la Magereza linaendelea na utekelezaji wa agizo la Serikali kuhusu Matumizi ya Nishati safi ya kupikia chakula cha Wafungwa na Mahabusu, ambapo mpaka kufikia Novemba 2024 Magereza kadhaa yameanza kutumia nishati safi ikiwemo Gereza Lilungu, Keko, Ukonga, Butimba, Ilagala, Babati, Isanga na Karanga huku maandalizi ya Miundombinu ya Biogas kwa Kambi Kimbiji na Ngara yakiendelea vizuri.

Pia CGP. Katungu amesema umesha fanyika Ununuzi wa jumla ya tani 167 za mkaa mbadala wa rafiki unao zalishwa na STAMICO  na kusambazwa katika Magereza 16, lengo likiwa ni kuwezesha matumizi ya Nishati safi, ambapo kwasasa tupo katika hatua ya ukamilishaji wa upatikanaji wa majiko kwa ajili ya utumiaji wa mkaa huo.

Aidha CGP. Katungu amesema, Jeshi la Magereza kwa kushirikiana na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) linaendesha program ya matumizi ya Nishati safi ya kupikia Magerezani ambayo inahusisha jumla ya Vituo 211 yakiwemo Magereza 129, Ofisi za Mikoa 26, vituo vya Magereza 04, Makao Makuu, Bohari Kuu, Hospitali Kuu ya Jeshi, Karakana, Bwawani Sekondari pamoja na Kikosi cha Kutuliza Ghasia na Kambi za Magereza takribani 47 pamoja na Watumishi wote wa Magereza wapatao 15,920.

Thursday, October 24, 2024

DKT. MPANGO AFUNGUA MKUTANO WA MWAKA WA MAAFISA WAANDAMIZI WA JESHI LA MAGEREZA

Na. SP. Kilian Ngalla - DODOMA


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Philip Isidor Mpango, leo tarehe 24 Oktoba, 2024 amefungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza ambapo Mkutano huo wa siku mbili unalenga kufanya tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya Jeshi la Magereza na kuweka mikakati ya kuboresha utendaji kazi. 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo Dkt. Mpango amesema, Jeshi la Magereza lishirikiane na Jeshi la Polisi pamoja na Bodi ya Taifa ya Parole ili kuweka utaratibu wa pamoja wa kuwatambua na kuwafuatilia wale wote wanaotoka Magerezani baada ya kumaliza vifungo vyao ili wawezeshwe kwa kupewa mikopo kutoka kwa Halmashauri zinazowazunguka itakayowasaidia kufanya biashara na kujikimu kimaisha ili kuwaepusha kurudi tena Magerezani.

Dkt. Mpango pia amesema, mchakato wa marekebisho ya Sheria ya Magereza ni mchakato muhimu lakini hautakua na maana iwapo Maafisa na askari hawatabadilika kimtazamo kuendana na mazingira, kwa kuwa Sheria na mifumo ya Magereza tuliyo nayo tumeirithi kutoka kwa wakoloni hivyo ameitaka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuharakisha marekebisho ya Sheria hiyo yanafanyika haraka na yazingatie mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai. 

Makamu wa Rais aliendelea kusisitiza kuwa mkutano huu usaidie kuleta mitazamo chanya ndani ya Jeshi la Magereza kuhusu mabadiliko na kujitosheleza kwa chakula ikiwa ni pamoja na kuzalisha miche na mbegu bora za mazao tofauti ya kimkakati ili kuondokana na utegemezi kutoka nje ya Nchi huku akisisitiza kuwa Viwanda vyetu vya ndani na vile vya ubia vinazalisha na kukidhi masoko ya ndani ya Nchi. 

“Ili kuendelea kuboresha kilimo na kujitosheleza kwa chakula Jeshi halina budi kununua au kukopa zana bora za kilimo kutoka taasisi binafsi ili kuzalisha chakula kwa aajili ya Wafungwa na Mahabusu” Alisema Dkt. Mpango.

Aidha Dkt. Mpango amelitaka Jeshi la Magereza lishirikiane na Wakala wa Misitu Tanzania ili kuweza kuzalisha miche ya miti na matunda ili liwe kielelezo cha utunzaji wa Mazingira.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh. Mhandisi Hamad Masauni amesema,ndoto ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuona Jeshi la Magereza linatumia rasilimali zake kikamilifu ikiwemo ardhi ili kuzalisha kwa tija na kujitosheleza kwa chakula na kutoa mchango kwa Taifa ili kutatua changamoto ndani ya Jeshi na kuipunguzia mzigo Serikali.

Naye Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP) Jeremiah Yoram Katungu amesema, mwelekeo wa Jeshi la Magereza ni kuhakikisha tunaboresha Programu za Urekebishaji wa Wafungwa ili ziendane na wakati uliopo na kwa kuzingatia Sheria za nchi, Kikanda na Kimataifa.

Aidha CGP. Katungu ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi inavyoliwezesha Jeshi la Magereza kutekeleza majukumu yake kwa kuliongezea bajeti, kuajiri askari wapya na kuwapandisha vyeo maafisa na askari katika ngazi mbalimbali wapatao 11,880 kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2020/2021 hadi mwaka 2023/2024.

Hafla ya ufunguzi wa mkutano wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza imehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali.

Wednesday, October 9, 2024

CGP. KATUNGU AMTEMBELEA MAKAMU WA RAIS DKT. MPANGO, OFISINI KWAKE

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP) Jeremiah Yoram Katungu, Oktoba 07, 2024 amemtembelea Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ofisini kwake jijini Dodoma, kwaajili ya kujitambulisha ikiwa ni mara ya kwanza tangu alipoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuliongoza Jeshi la Magereza hivi karibuni.




Friday, October 4, 2024

WAZIRI MASAUNI AFANYA ZIARA MAGEREZA MAKAO MAKUU, AKUTANA NA MENEJIMENTI YA SHIMA.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mhandisi Hamad Masauni (Mb), Oktoba 04, 2024 amefanya ziara ya kikazi Makao Makuu ya Magereza Msalato jijini Dodoma na kufanya Kikao na Menejimenti ya Shirika la Uzalishaji Mali Jeshi la Magereza (SHIMA) Pamoja na Wakuu wa Magereza Mikoa na Wakuu wa Vituo vya Magereza vinavyo tekeleza Miradi mbalimbali ya Shirika hilo.


Katika kikao hicho yamejadiliwa mambo mbalimbali ikiwemo utendaji wa Shirika na mikakati ya kulifanya lizalishe zaidi kwa manufaa ya Jeshi la Magereza na Taifa kwaujumla, 


Kikao hicho pia kimedhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Danniel Sillo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Maduhu Kazi, Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP) Jeremiah Yoram Katungu na Maafisa Waandamizi wa Magereza Makao Makuu.

TCTA YAKABIDHIWA GARI MPYA KWA SHUGHULI ZA UTAWALA.

Na. A/insp. Nurdin Nanyanga.


Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Sayansi ya  Urekebishaji Tanzania (TCTA) kilichopo Ukonga jijini Dar es salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza (SACP) Willington Kahumuza, Mapema leo Oktoba 04, 2024 amekabidhiwa gari mpya aina ya Toyota Land Cruiser Hard top na Mkuu Msaidizi  wa Kitengo cha Usafirishaji cha Jeshi la Magereza Mrakibu wa   Magereza (SP) Adam Kipalamoto, kwaniaba ya Kamishna Jenerali wa Magereza Jeremiah Yoram Katungu.


Akizungumza wakati wa makabidhiano ya gari hilo , Mkuu wa Chuo SACP. Kahumuza amemshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzani Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuliwezesha Jeshi la Magereza vitendea kazi.


Aidha amemshukuru Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni (MB) na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP) Jeremiah Yoram Katungu kwa kuwapa kipaumbele kwa Chuo TCTA katika Mgao wa gari

Aidha amewataka Watumishi wa Chuo kulitunza gari hilo ili liweze kudumu na kufanya kazi zilizokusudiwa.



CGP. KATUNGU AFANYA KIKAO NA WATENDAJI WA SHIMA JIJINI DODOMA.


Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP) Jeremiah Katungu,  Oktoba 03, 2024 amekutana na Watendaji wa Shirika la Uzalishaji Mali Jeshi la Magereza (SHIMA) wakiongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Shirika hilo, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Omary Msepwa, kwaajili kujadili masuala mbalimbali ya kiutendaji wa Shirika hilo ili liweze kuleta tija zaidi katika Uzalishaji.




DPP. MWAKITALU ATEMBELEA MAGEREZA MAKAO MAKUU, AFANYA MAZUNGUMZO NA CGP. KATUNGU.


Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP) Jeremiah Katungu, amekutana na kuzungumza na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) Silvester Mwakitalu, alipotembelea Makao Makuu ya Magereza Msalato, jijini Dodoma, Oktoba 03, 2024.


CGP. KATUNGU AKUTANA NA KUZUNGUMZA NA WAZIRI WA FEDHA DKT. MWIGULU NCHEMBA.


Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP) Jeremiah Yoram Katungu, Oktoba 03, 2024 ambetembelea Ofisi za Wizara ya Fedha zilizopo Jijini Dodoma, ambapo amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb).


Lengo la ziara hiyo ni kujitambulisha na kujadili masuala mbalimbali ikiwemo mipango ya maendeleo ya Jeshi la Magereza.

Kamishna Jenerali wa Magereza Jeremiah Yoram Katungu, akiagana na Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, mara baada ya mazungumzo yao, jijini Dodoma, Octoba 03, 2024


KATIBU MKUU WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI AFANYA ZIARA MAGEREZA MAKAO MAKUU, AZINDUA MAGARI MAPYA 11

 Na. Sgt. Geofrey Jacka - DODOMA


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ndg. Ally Senga Gugu, akikata utepe kuashiria Uzinduzi wa Magari 11 ya Jeshi la Magereza.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ndg. Ally Senga Gugu, leo Oktoba 02, 2024 ametembelea Makao Makuu ya Jeshi la Magereza eneo la Msalato Jijini Dodoma na  kupokelewa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Jeremiah Y Katungu, pamoja na maafisa wa ngazi mbalimbali.


Akizungumza na Maafisa, Askari na Watumishi wasio Askari Katibu Mkuu Gugu amesema, lengo la ziara hiyo ni kujitambulisha ili kufahamiana na kupeana Miongozo ya kiutendaji wa kazi huku akiahidi Ushirikiano na Viongozi wa Jeshi la Magereza katika kutatua changamoto zinazowakabili watumishi na kusisitiza umoja na ushirikiano miongoni mwa watendaji. 


Aidha Ndg. Gugu ameutaka Uongozi wa Jeshi la Magereza kutumia falsa ya 4R ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inabeba  Ujumbe wa Maridhiano (Reconcilation)  Ustahamiliivu (Resilience) Mabadiliko (Reforms) na Kujenga Upya yaani Rebuilding, ambayo imeonesha mafanikio  makubwa pale inapotekelezwa kikamilifu.


Kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu kuzungumza, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP) Jeremiah Katungu alitoa maelezo ya kina kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na Jeshi la Magereza nchini na kumshukuru Katibu Mkuu Kwa kutenga muda wake kufanya ziara ndani ya Jeshi la Magereza.


Katibu Mkuu Ndg. Ally Senga Gugu pia alipata fursa ya kuzindua Magari 11 ya Jeshi la Magereza yatakayo tumika katika shughuli za kiutawala, pamoja na gari moja la kubebea wagonjwa (Ambulance ) ambalo litapelekwa Hospitali Kuu ya Jeshi la Magereza iliyopo Ukonga, Jijini Dar es Salaam.