Saturday, October 17, 2015

Mahafali ya kidato cha nne shule ya sekondari Bwawani inayomilikiwa na Jeshi la Magereza yafana mkoani Pwani

Mgeni rasmi Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Mbarak Abdulwakil akimkabidhi cheti Mwanafunzi Mhitimu kwenye Mahafali ya Kumi na mbili ya Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Bwawani Oktoba 16, 2015(kulia kwa Mgeni rasmi) ni Kamishna Jenerali wa Magereza, John Casmir Minja.
Baadhi ya Wahitimu Kidato cha Nne Shule ya Sekondari Bwawani inayomilikiwa na Jeshi la Magereza wakipiga makofi wakati wa hotuba ya Mgeni rasmi Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mbarak Abdulwakil(hayupo pichani).
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Mbarak Abdulwakil(katikati) akiwa na Viongozi mbalimbali Meza Kuu wakiimba wimbo wa Shule ya Sekondari Bwawani kwenye hafla ya Mahafali ya Kidato cha Nne ya shule hiyo(wa pili kushoto) ni Kamishna Jenerali wa Magereza, John Casmir Minja(wa pili kulia) ni Mwenyekiti wa Bodi ya Shule, Kamishna wa Magereza wa Utawala na Fedha, Gaston Sanga
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Mbarak Abdulwakil(kulia) akisoma jiwe la msingi la Jengo la Maabara ya masomo ya Sayansi kama anavyoonekana katika picha.
Muonekano wa nje wa Jengo la Maabara ya Masomo ya Sayansi katika Shule ya Sekondari ya Bwawani baada ya Mgeni rasmi kuweka jiwe la msingi.
Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja akitoa maelezo mafupi kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi kwenye Mahafali ya Kidato cha Nne Shule ya Sekondari Bwawani.
Baadhi ya Walimu na Wafanyakazi wa Shule ya Sekondari Bwawani wakifuatilia kwa makini maelezo ya Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza kwenye Mahafali hayo ya Kidato cha Nne.
Wahitimu wa kidato cha nne katika shule ya Sekondari Bwawani wakigani shairi lao mbele ya Mgeni rasmi.Na Lucas Mboje, Pwani

Wahitimu wa kidato cha nne nchini wameaswa kuachana na fikria potofu kuwa elimu wanayoipata itawapatia ajira Serikalini au kwenye Sekta binafsi badala yake watumie elimu hiyo kama nyenzo muhimu ya kuwawezesha kujiajiri wao wenyewe.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi, Bw. Mbarak Abdulwakil alipokuwa mgeni rasmi wakati wa mahafali ya kumi na mbili ya kidato cha nne katika shule ya Bwawani Sekondari iliyopo Mkoani Pwani.

"Katika hali ya sasa ya utandawazi yapo mambo kadhaa ambayo mtu binafsi anaweza kuyafanya na kujipatia kipato cha kujiendeleza maisha yake". Alisema Bw. Abdulwakil.

Bw. Abdulwakil amesisitiza kuwa wanachotakiwa kufanya wahitimu hao ni kuyasoma mazingira ya maisha popote watakapokuwa na kuamua namna ya kujiajiri ili mradi isiwe shughuli zinazopingana na sheria na maadili ya kijamii, kama vile kuuza madawa ya kulevya, ukahaba, unyang'anyi na mambo mengine yanayofanana na hayo.

Awali akimkaribisha Mgeni rasmi Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja alisema kuwa uongozi wa Jeshi la Magereza kwa kushirikiana na Bodi ya shule utaendelea kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazozikabili shule hiyo kadri uwezo wa kifedha unavyopatikana.

Jeneral Minja alizitaja baadhi ya changamoto mbalimbali ambazo tayari zimefanyiwa kazi ikiwemo miradi ya miundo mbinu ya msingi kama vile Madarasa, Maabara, Maktaba na mradi wa maji ambapo kwa kiasi kikubwa miradi hiyo imechangia kuboresha maendeleo ya kitaaluma shuleni hapo.

Kwa upande wake Mkuu wa shule ya Sekondari Bwawani, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Emmanuel Lwinga alipokuwa akitoa taarifa fupi kwa mgeni rasmi katika mahafali hayo amesema kuwa shule yake ni miongoni mwa shule nchini ambazo zinafanya vizuri kitaaluma na masuala mengineyo yasiyoyakitaaluma.

Aliongeza kuwa mwaka 2014 kati ya wanafunzi 95 waliofanya mitihani ya kidato cha nne katika shule hiyo wanafunzi 87 sawa na asilimia 91.6% walifaulu, aidha wanafunzi 52 walichaguliwa kujiunga na masomo ya Kidato cha Tano katika shule mbalimbali za serikali.

Shule ya Sekondari Bwawani inamilikiwa na Jeshi la Magereza, ilianzishwa Mwaka 1978 kwa lengo la kutoa elimu ya Sekondari kwa Watumishi wa Magereza ambapo hivi sasa shule hiyo inatoa elimu kwa vijana wa kike na kiume kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita.