Saturday, January 30, 2016

Naibu katibu mkuu wizara ya mambo ya ndani ya nchi atembelea mradi wa umwagiliaji gereza la kilimo Idete, mkoani Morogoro

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani, Mhe. Balozi Simba Yahya akisalimiana na Maafisa wa Jeshi la Magereza mara baada ya kuwasili gerezani hapo kwa ziara ya kikazi Januari 29, 2016 kujionea ujenzi wa mradi wa umwagiliaji Gereza la Kilimo Idete lililopo Wilaya ya Kilombero, Mkoani Morogoro(anayefuatia) ni Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, Dkt. Juma Malewa.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Balozi Simba Yahya(wa pili kulia) akiwa ameongozana na Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(wa kwanza kushoto) kuelekea katika Ukumbi wa Gereza hilo kwa ajili ya kupata taarifa kamili ya utekelezaji wa mradi wa umwagiliaji Gereza la Kilimo Idete kutoka kwa Wakandarasi wa mradi na Mshauri Mwelekezi mradi(kulia) ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilombero, Bw. Yahya Sinaniya.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Balozi Simba Yahya akiangalia sehemu ya banio la kutunzia maji ya mradi wa Gereza la Kilimo Idete akiwa pamoja na msafara wa Wajumbe wa Bodi ya Zabuni ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi(wa kwanza kushoto) ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Manunuzi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Manyama Mapesi(wa pili kushoto) ni Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, Dkt. Juma Malewa.
Muonekano wa mfereji wa maji yatakayokuwa yakitumika katika mradi wa umwagiliaji wa Gereza la Kilimo Idete, Mkoani Morogoro kama inavyoonekana katika picha.
Mshauri wa Mradi, Mhandisi Nzobonaliba Imani akiteta jambo na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Balozi Simba Yahya(katikati) alipotembelea mradi wa umwagiliaji wa Gereza la Kilimo Idete lililopo Mkoani Morogoro(kulia) ni Mkuu wa Gereza hilo, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza, Nsajigwa Mwakenja wakiaangalia ujenzi wa mradi wa umwagiliaji wa Gereza hilo.
Wakandarasi wa Kampuni ya ujenzi wa mradi wa umwagiliaji wa Gereza Kilimo Idete, lililopo Mkoani Morogoro wakiendelea na ujenzi wa mifereji ya maji kama inavyoonekana katika picha.
Wajumbe wa Bodi ya Zabuni ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wakipata maelezo ya Kitaalam kutoka kwa Mshauri Mwelekezi walipotembelea mradi huo kujionea hatua mbalimbali za ujenzi. Wengine ni Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya ya Kilombero.


Na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza, Morogoro

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Balozi Simba Yahya amemtaka Mkandarasi wa Kampuni ya "Tanzania Building Works ya Jijini, Dar es Salaam" inayojenga mradi wa umwagiliaji Gereza la Kilimo Idete kuukamilisha mradi huo katika muda walioongezewa ili kuwezesha kuanza kwa shughuli za uzalishaji gerezani hapo.

Akizungumza na Wakandarasi wa Kampuni hiyo alipofanya ziara ya kikazi Gereza Idete, Balozi Yahya amesema kuwa kukamilika kwa mradi huo ni mkombozi kwa Jeshi la Magereza kwani utawezesha uzalijashi wa chakula cha kutosha cha wafungwa waliopo magerezani pamoja na kuzalisha ziada itakayouzwa kwa Wananchi ili kuongeza Mapato Serikalini.

"Ni matarajio yangu kuwa Mkandarasi wa Mradi huu kwa kushirikiana na Mshauri Mwelekezi na Wadau wa Jeshi la Magereza atakamilisha mradi huu kwa wakati kama alivyotuahidi hivyo kuanza mara moja shughuli za uzalishaji". Alisisitiza Balozi Yahya.

Naye Msimamizi wa mradi huo Mhandisi Lodia Mallion alisema kuwa mradi huo umekamilika kwa asilimia 60 ambapo tayari uchimbaji na ujenzi wa mifereji itakayokuwa ikipitisha maji kwenda mashambani imekwisha kukamilika.

"Mito inayotumika kama vyanzo vya maji ni mto Kilombero pamoja na mto Kiwiliwili ambapo banio linalotunza maji kwa shughuli za umwagiliaji tayari limekamilika". Alisikika Mhandisi Mallion.

Awali Mkuu wa Gereza Idete, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza, Nsajigwa Mwakenja akiwasilisha taarifa kwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Balozi Yahya amesema kuwa kazi ya kuandaa mradi huu ilianza rasmi mwaka 2013 ambapo mradi huo unatarajiwa kukamilika Mwaka huu 2016 ambapo gharama za mradi huo zinakadiriwa kufikia kiasi cha Tsh. 2.5 Bilioni.

Aidha amesema kuwa chakula kitakachopatikana katika mradi huo wa Gereza Idete kitatumika kulisha wafungwa waliopo magerezani na ziada itakayopatikana itauzwa kwa Wananchi hivyo kuongeza pato la Taifa.

Gereza la Kilimo Idete lipo Wilayani Kilombero, Mkoani Morogoro linajishughulisha na Kilimo cha mpunga wa chakula na pia mpunga kwa ajili ya mbegu bora za Kilimo hapa nchimi. Gereza hilo lilianzishwa rasmi mwaka 1983 kwa ajili ya Kilimo cha mazao mbalimbali hususani Kilimo cha mpunga.