Friday, April 22, 2016

Wahitimu Bwawani Sekondari waaswa kuwa waadilifu na wazalendo kwa Taifa

Mgeni rasmi Kamishna wa Fedha na Utawala wa Magereza, Gaston Sanga akitoa cheti kwa mwanafunzi mhitimu wa kidato cha sita katika mahafali ya kwanza ya kidato cha sita Bwawani Sekondari, yaliyofanyika leo Aprili 22, 2016.

Mkuu wa shule ya Bwawani Sekondari, ACP.  Emmanuel Lwinga akitoa maelezo mafupi ya maendeleo ya shule kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kutoa hotuba yake.
Wanafunzi wahitimu wa Kidato cha sita Bwawani Sekondari wakiimba wimbo wa shule kwenye mahafali hayo yaliyofanyika leo Aprili 22, 2016, Mkoani Pwani.
Kamishna wa Utawala na Fedha, Gaston Sanga akiwasalimu wahitimu na wazazi kabla ya kutoa hotuba fupi kwa wahitimu wa kidato cha sita Bwawani Sekondari(hawapo pichani).

Wazazi wa wahitimu wa kidato cha sita shule ya Bwawani Sekondari wakifuatilia kwa makini hotuba ya Mgeni rasmi
Ujenzi wa Bweni la Wasichana katika shule ya Bwawani Sekondari ukiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi kama inavyoonekana katika picha.
 
Mgeni rasmi Kamishna wa Fedha na Utawala wa Magereza, Gaston Sanga(katikati)akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wahitimu kidato cha sita Bwawani Sekondari(waliosimama mstari wa nyuma)mahafali hayo yamefanyika leo Aprili 22, 2016

(Picha zote na lucas mboje wa Jeshi la Magereza).


Na Lucas Mboje, Pwani

WAHITIMU wa Kidato cha sita nchini wameaswa kuwa waadilifu na wazalendo ili hatimaye taifa liweze kupata viongozi bora na raia wema katika jamii.

Rai hiyo imetolewa na Kamishna wa Fedha na Utawala wa Magereza Gaston Sanga  akiongea kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini katika mahafali ya kwanza ya Kidato cha sita ya Shule ya Bwawani Sekondari iliyopo Mkoani Pwani.

“Nadhani wote ni mashahidi kwa namna Serikali ya Awamu ya Tano inavyowahudumia wananchi kwa kasi na kiwango cha kuridhisha. Hivyo mkipata kazi nawasihi mkawajibike kwa kasi, uadilifu na mkawe wazalendo kwa taifa”. Alisema Kamishna Sanga.

Kamishna Sanga ameongeza kuwa kwa kufanya hivyo watakuwa wameunga mkono kwa vitendo juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Aidha, Afande Sanga ameahidi kuwa Uongozi wa Jeshi la Magereza kwa kushirikiana na Bodi ya shule hiyo utaendelea kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazozikabili shule hiyo kadri uwezo wa kifedha unavyopatikana.

Kwa upande wake Mkuu wa shule ya Sekondari Bwawani, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Emmanuel Lwinga alipokuwa akitoa taarifa fupi kwa mgeni rasmi katika mahafali hayo amesema kuwa shule yake ni miongoni mwa shule bora nchini ambazo zinafanya vizuri kitaaluma na masuala mengineyo yasiyoyakitaaluma.

Aliongeza kuwa katika mitihani mbalimbali waliyofanya wanafunzi hao wa kidato cha sita wamekuwa na matokeo mazuri kutokana na mazingira mazuri ya kujisomea, ushirikiano mzuri wa walimu pamoja na kuimarishwa kwa miundombinu muhimu ya kujifunzia.

"Afande mgeni rasmi wanafunzi wahitimu 13 wa leo tuna hakika kuwa watatuletea matunda mazuri kutokana na mwelekeo waliouonesha katika mitihani ya ndani na nje ya shule waliyoifanya". Alisema Mkuu wa Shule Lwinga.

Shule ya Sekondari Bwawani inamilikiwa na Jeshi la Magereza, ilianzishwa Mwaka 1978 kwa lengo la kutoa elimu ya Sekondari kwa Watumishi wa Magereza ambapo hivi sasa shule hiyo inatoa elimu kwa vijana wa kike na kiume kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini kuanzia kidato cha kwanza hadi cha Sita.