Friday, March 11, 2016

Ziara ya Kamishna Jenerali wa Magereza nchini mkoani Kagera

Kamishna Jenerali wa Magereza John C. Minja( wa pili kushoto) akikagua maeneo mbalimbali ya Gereza Bukoba alipofanya ziara ya kikazi leo Machi 11, 2016 (wa kwanza kushoto) ni Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kagera, SACP. Omari Mtiga (wa pili kulia) ni Mkuu wa Gereza Bukoba, ACP. Benizeth Bisibe.
Kamishna Jenerali wa Magereza John C. Minja (wa nne kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Maofisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza Mkoani Kagera mara baada ya kutembelea Gereza la Wilaya ya Bukoba 
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. John Mongella akiongea ofisini kwake na Kamishna Jenerali wa Magereza John C. Minja na ujumbe wake (hawapo pichani)
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. John Mongella akiongea ofisini kwake na Kamishna Jenerali wa Magereza John C. Minja na ujumbe wake kama inavyoonekana katika picha.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba Mhe. Sivangilwa Mwangesi Akisalimiana na Kamishna Jenerali wa Magereza John C. Minja alipomtembelea ofisini kwake

(Picha na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).


Kamishina Jenerali wa Mageraza nchini John Carmir Minja afanya ziara ya kikazi  Mkoani Kagera yenye lengo la kutembelea na kukagua Magereza ya Mkoa wa Kagera pamoja na kujionea miradi ya uzalishaji inayosimamiwa na Jeshi hilo.

Akiwa Mkoani hapa Kamishna Jenerali Minja alifika ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. John Mongella na kufanya naye mazungumzo kuhusu utendaji kazi na ufanisi wa Jeshi la Magereza Mkoani hapa katika kuimarisha ulinzi na usalama.

Aidha katika mazungumzo hayo walizungumzia  changamoto ya  msongamano wa Mahabusu katika Gereza la Wilaya ya Muleba ambalo hivi sasa linatumika kuhifadhi Mahabusu wa Wilaya ya Muleba na Wilaya ya Chato Mkoani Geita ambayo haina Gereza la Wilaya.

Kamishna Jenerali wa Mageraza nchini John Carmir Minja pia alitembelea Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba na kufanya mazungumzo na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo Mhe. Sivangilwa Mwangesi juu ya namna ya kuongeza kasi ya usikilizwaji wa kesi mbalimbali za watuhumiwa ili kuondoa msongamano Magerezani.

Vilevile Kamishna Jenerali Minja alitembelea Gereza la Wilaya la Bukoba na kuongea na wafungwa na Mahabusu wa Gereza  hilo pia na kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la zahanati ambalo lipo katika hatua za mwisho kukamilishwa ili liweze kutoa huduma za afya kwa wafungwa na watumishi wa Jeshi hilo pamoja na wananchi wanaoishi jirani na zahanati hiyo.

Kamishna Jenerali Minja yupo Mkoani Kagera kwa siku 7 kuanzia tarehe 10 hadi 16 Machi, 2016 ambapo lengo la ziara hiyo ni kutembelea na kukagua Magereza ya Mkoa wa Kagera pamoja na kujionea miradi ya uzalishaji inayosimamiwa na jeshi hilo.