Friday, January 27, 2017

JESHI LA MAGEREZA, PPF NA NSSF KUITIKIA TANZANIA YA VIWANDA KWA VITENDO

Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza Dkt. Juma Malewa (mwenye miwani) na ujumbe wake wakiwasili Gereza Mbigiri Mkoani Morogoro jana tarehe 26.01.2017 tayari kwa kukagua eneo la uwekezaji wa Kilimo cha Miwa na Uzalishaji wa Sukari. Wa kwanza nyuma yake ni Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Prof.Godius  Kahyarara, mshauri mwelekezi katika mradi huo ndugu  Seleman Karanga akifuatiwa na Mkurugenzi Mkuu wa PPF ndugu William Erio
Ujumbe wa Uwekezaji wa Ubia katika kiwanda cha sukari cha Mbigiri kati ya  Mifuko ya Jamii ya NSSF, PPF na Jeshi la Magereza  kupitia Shirika la Magereza (Corporation Sole) wakikagua baadhi ya maeneo ya ndani ya kiwanda cha zamani cha sukari cha Gereza hilo kilichosimamisha uzalisha zaidi ya miaka 10 iliyopita.
Ujumbe wa Uwekezaji wa Ubia katika kiwanda cha sukari cha Mbigiri kati ya  Mifuko ya Jamii ya NSSF, PPF na Jeshi la Magereza wakipata  maelezo kutoka kwa Mrakibu Msaidizi wa Magereza (ASP) Angolwise Pilla (wa pili kushoto) ambaye ni mfanyakazi wa zamani kilichokuwa kiwanda cha sukari cha Gereza Mbigiri kilicho simamisha uzalisha zaidi ya miaka 10 iliyopita.
Viongozi waandamizi kutoka Jeshi la Magereza, PPF na NSSF wakipata maelezo ya namna kiwanda cha sukari cha Gereza Mbigiri mkoani Morogoro kilivyokuwa kikifanya kazi kutoka kwa mfanyakazi wa zamani wa kiwanda hicho  Mrakibu Msaidizi wa Magereza (ASP) Angolwise Pilla (wa nne kushoto). Viongonzi hao walitembelea kiwanda hicho jana ikiwa ni hatua za awali za uwekezaji wa ubia katika uzalishaji wa sukari nchini kati ya Taasisi hizo tatu.
Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza Dkt. Juma Malewa (wa pili kushoto) akisikiliza kwa makini maelezo na namna kiwanda cha zamani cha sukari cha Gereza Mbigiri mkoani Morogoro kilivyokuwa kikifanya kazi kutoka kwa mmoja wa wafanyakazi wa zamani wa kiwanda hicho Mrakibu Msaidizi wa Magereza (ASP) Angolwise Pilla (wa pili kuli). Nyuma ya Dr. Malewa ni Mkurugenzi Mkuu wa PPF William Erio na  wa tatu ni Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa NSSF Prof. Godius Kahyarara.
Mwonekano wa baadhi ya majengo ya kilichokuwa kiwanda cha sukari cha Gereza Mbigiri Mkoani Morogoro. Kiwanda hicho kilisimamisha uzalishaji tangu mwaka 1996 kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uchakavu wa mitambo. Mifuko ya PPF, NSSF na Jeshi la Magereza wako katika hatua za awali za kuingia ubia wa kufufua Kiwanda hicho ili kuitikia kauli mbiu ya serikali ya Awamu ya Tano inayotilia msisitizo wa ujenzi wa viwanda.
Msafara wa wawekezaji wa ubia kati ya Mifuko ya PPF, NSSF na Jeshi la Magereza katika Kiwanda cha Sukari katika Gereza la Mbigiri Mkoani Morogoro wakikagua eneo la mashamba yatakayolimwa miwa kwa ajili ya kiwanda hicho. Eneo la ekari 12,000 zimetengwa kwa ajili ya kuanza kilimo cha miwa.
Mkuu wa Gereza la Mbigiri Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Charlez Kimbi (aliyeinua mkono juu) akitoa ufafanuzi wa jambo katika ziara ya kukagua shamba la hekari 12,000 zilizotayari kwa kilimo cha miwa kwa ajili ya uzalishaji wa sukari.
Maafisa wa Jeshi la Magereza, PPF na NSSF wakipiga kambi polini ili kuteta jambo wakati wa ziara ya kukagua shamba linalotarajiwa kulimwa miwa kwa ajili ya kiwanda cha sukari cha Gereza Mbigiri kinachotarajiwa kuendeshwa kwa ubia wa Taasisi hizo tatu.
Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza Dkt. Juma Malewa akifafanua jambo kwa waandishi wa habari wakati wa ziara ya kutembelea eneo la uwekezaji wa Kilimo cha Miwa na Uzalishaji wa sukari mradi utakaoendeshwa kwa ubia kati ya Jeshi la Magereza kupitia Shirika la Magereza (Corporation Sole), Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya PPF na NSSF katika eneo la Gereza Mbigiri Mkoani Morogoro, jana tarehe 26. 01. 2017
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Jamii wa PPF ndugu William Erio akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari wakati wa ziara ya kutembelea eneo la uwekezaji wa Kilimo cha Miwa na Uzalishaji wa sukari mradi utakaoendeshwa kwa ubia kati ya Jeshi la Magereza kupitia Shirika la Magereza (Corporation Sole), Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya PPF na NSSF katika eneo la Gereza Mbigiri Mkoani Morogoro, jana tarehe 26. 01. 2017
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Jamii wa NSSF Prof.Godius Kahyarara akitoa maelezo ya ziada  kwa waandishi wa habari wakati wa ziara ya kutembelea eneo la uwekezaji wa Kilimo cha Miwa na Uzalishaji wa sukari mradi utakao endeshwa kwa ubia kati ya Jeshi la Magereza kupitia Shirika la Magereza (Corporation Sole), Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya PPF na NSSF katika eneo la Gereza Mbigiri Mkoani Morogoro, jana tarehe 26. 01. 2017

(Picha zote na ASP Deodatus Kazinja, PHQ) 

Na ASP Deodatus Kazinja, Magereza Makao Makuu
Katika kuitikia wito wa serikali ya Awamu ya Tano wa Kujenga Tanzania ya Viwanda Jeshi la Magereza kupitia Shirika la Magereza (Corporation Sole) limeingia ubia na Mifuko ya Jamii ya PPF na NSSF wa kufufua kilichokuwa kiwanda cha Sukari kilichopo Gereza Mbigiri Mkoani Morogoro.
 
Kiwanda cha sukari cha Mbigiri kilisimisha uzalishaji tangu mwaka 1996 kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uchakavu wa mitambo. Lakini kutokana na kuwa eneo zuri kimkakati yaani uwepo wa raslimali ardhi ya kutosha, nguvu kazi ya baadhi ya wataalam wa zamani wa kiwanda hicho, chanzo cha maji kuwezesha kuendesha kilimo cha umwagiliaji kumezishawishi taasisi zingine kushirikiana na Jeshi la Magereza kuwekeza katika eneo hili.
 
Akiongea na waandishi wa habari katika ziara ya kukagua eneo la Uwekezaji Kaimu Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Dkt. Juma Malewa amesema uwekezaji huu utakuwa na faida nyingi ikiwa ni pamoja na kuongeza ajira, upatikanaji wa sukari ya kutosha nchini lakini pia wakulima  wa eneo hilo watapata soko la uhakika la kuuza miwa katika kiwanda hicho.
 
Aidha Kaimu Kamishna huyo ametoa wito kwa wananchi kutovamiwa maeneo ya majeshi kwani mengi yamehifadhiwa kwa shughuli za baadae zenye maslahi mapana kwa taifa.
 
Naye Mkurugenzi Mkuu wa PPF William Erio amesema matarajio yao ni kuona kiwanda kinaanza mapema iwezekanavyo hivyo, ametoa wito kwa wananchi wa maeneo jirani kuchangamkia fursa ya kulima zao la miwa kwa maana sasa watakuwa na uhakika wa soko lililo karibu nao.
 
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Prof. Godius Kyaharara amesema kuwa kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 30,000 kwa mwaka na kitahitaji tani 500,000 za miwa hivyo ni fursa nzuri kwa wananchi wa maeneo jirani.
 
“Ni matarajio yetu kuwa kiwanda hiki kitaongeza ajira, kitainua uchumi kwa wafanyakazi na wanakijiji, tutapata wanachama wengi zaidi lakini pia tutakuwa tumeongeza uwezo wetu vizuri zaidi wa kuwahudumia wanachama wetu kupitia uwekezaji huu” Alihitimisha Prof. Kahyarara.