Sunday, January 29, 2017

KAIMU KAMISHNA JENERALI WA MAGEREZA DR. JUMA MALEWA AHITIMISHA ZIARA MAGEREZA MKOANI MOROGORO NA PWANI

Kaimu Mkuu wa Magereza Mkoa wa Morogoro  Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP)Mzee Nyamka akitoa taarifa ya utendaji katika mkoa wake kwa Kaimu Kamishna Magereza Dr. Juma Malewa (hayupo pichani) mwishoni mwa juma hili alipofanya ziara ya kiutendaji katika baadhi ya Magereza mkoani humo.
Baadhi ya Maafisa na askari wa Gereza Mbigiri Mkoani Morogoro wakifuatilia ufafanuzi wa hoja mbalimbali walizozitoa mbele ya Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza Dr. Juma Malewa (hayupo pichani) alipofanya ziara kituoni hapo na kufanya Baraza la watumishi hao ili kusikiliza kero, hoja na mapendekezo yote ikiwa ni kuboresha utendaji kazi wa siku kwa siku.
Baadhi ya Maafisa na askari wa Gereza  Wami Kuu pamoja na Wami Vijana Mkoani Morogoro kwa pamoja  kwa makini wakifuatilia ufafanuzi wa hoja mbalimbali walizozitoa kwa Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza Dr. Juma Malewa (hayupo pichani) katika Baraza la pamoja alipowatembelea hivi karibuni kuona utendaji kazi katika vituo vyao lakini pia kuwapa hamasa ya utendaji kazi.
Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza Dr. Juma Malewa (wa kwanza kulia) akitembelea jengo la Karakana ya Ufundi ya Gereza Wami Vijana.  Jengo hilo pamoja na kuendelea kutumika lakini bado linahitaji kukamilishwa kujengwa na kuwekewa miundombinu ili liweze kutoa huduma kama ilivyokusudiwa.
Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza Dr. Juma Malewa (katikati) akipata maelezo mafupi ya kiutendaji kutoka kwa Mkuu wa Gereza la Mahabusu Mrakibu wa Magereza (SP) Zephania Neligwa (aliyesimama) ofisini kwake wakati wa ziara ya Kaimu Kamishna Jenerali Mkoani Morogoro aliyoifanya mwishoni  mwa juma.
Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza Dr. Juma Malewa (wa kwanza kushoto) akitolea ufafanuzi hoja mbalimbali zilizotolewa na baadhi ya Maafisa na Askari katika kikao kilichojumuisha askari wa Ofisi ya Mkuu wa Magereza  Mkoa wa Morogoro na Gereza Mahabusu. 
Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza Dr. Juma Malewa (katikati)akisisitiza jambo wakati wa kikao  kikao chake kilichojumuisha askari wa Ofisi ya Mkuu wa Magereza  Mkoa wa Morogoro na Gereza Mahabusu. Kushoto ni Kaimu Mkuu wa Magereza Mkoa wa Morogoro Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Mzee R.Nyamka. Na kulia Mkuu wa Shirika la Magereza (Corporation Sole) Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Joel Bukuku na nawa mwisho ni Mkuu wa Kitengo cha Uwekezaji na Ujasiliamari wa Jeshi la Magereza Mrakibu Mwandamizi wa Magereza (SSP) Uswege Mwakahesya.
Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza Dr. Juma Malewa akisaini kitabu cha wageni ofisini kwa Mkuu wa Gereza Kihonda mara alipowasili kituoni hapo kujionea shughuli mbalimbali kituoni hapo  sanjari na kuongea na maafisa na askari wa kituo hicho mwishoni mwa Juma hili.
Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza Dr. Juma Malewa (wa kwanza kushoto) akikagua maendeleo ya jengo jipya la ofisi ya Mkuu wa Gereza Kihonda. Jengo hilo linashengwa kwa jitihada za Mkuu wa Gereza hilo kwa kushirikiana na maafisa na askari wa kituo hicho. Viongozi wengine hapo ni Kaimu Mkuu wa Magereza Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Mzee Nyamka, Mkuu wa Shirika la Magereza (Corporation Sole) Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Joel Bukuku na Mkuu wa Gereza Kihonda Kamishna Msaidizi wa Magereza Ben Mwansasu.
Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza Dr. Juma Malewa akiendelea kusikiliza hoja mbalimbali za maafisa na askari wa Gereza Kihonda wakati wa ziara ya kikazi kituoni hapo. Aliyesimama ni Mkaguzi Msaidizi wa Magereza (A/Insp) Amani Moses akichangia jambo wakati wa kikao hicho.
Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza Dr. Juma Malewa akisalimiana na baadhi ya maafisa wa gereza Kihonda mara alipowasili akiwa tayari kufanya kikao na watendaji wa gereza hilo.
Mmoja wa askari wa gereza Kihonda akiwa na sura ya bashasha baada ya kupata fursa ya kusalimiana na Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza mara baada ya kikao wakati wa ziara ya Kaimu Kamishna Jenerali katika baadhi ya vituo mkoani Morogoro ikiwemo gereza Kihonda, mwishoni wa juma hili
Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza Dr. Juma Malewa akikagua maendeleo ya moja ya nyumba za zinazojengwa kwa mtindo wa kujitolea katika gereza la Wanawake Kingolwira mkoani Morogoro ikiwa ni jitihada za kukabiliana na tatizo la uhaba wa nyumba kituoni hapo. Aliyefuatana naye ni Mkuu wa Gereza la Wanawake Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Loyce Luhembe
Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza Dr. Juma Malewa (katikati) akitolea ufafanuzi wa jambo katika kikao chake na watumishi wa gereza Kihonda alipofanya ziara ya kiutendaji katika baadhi ya Magereza ya mkoa wa Morogoro. Kushoto ni Kaimu Mkuu wa Magereza mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Mzee Nyamka na kulia Mkuu wa Gereza la Kihonda, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Ben Mwansasu.
Baadhi ya Maafisa na askari wa Kingolwira Complex inayojumuisha Chuo cha Uhunzi na Udereva, Gereza Mtego wa Simba, Gereza Mkono wa Mara na Gereza la Wanawake Kingolwira katika kikao cha pamoja na Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza Dr. Juma Malewa alipofanya ziara katika vituo hivyo kujionea shughuli mbalimbali za kila siku.
Sehemu ya Maafisa na askari wa vituo vya Bwawani Sekondari (inayomilikiwa na Jeshi la Magereza) na Gereza Ubena mkoani Pwani wakiwa katika kikao cha pamoja na Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza Dr. Juma Malewa (hayupo pichani) alipofanya ziara vituoni hapo ili kujionea shughuli za vitu hivyo lakini pia kusiliza shida na maoni ya watumishi katika vituo hivyo jana tarehe 28.01. 2017.
Mkuu wa Magereza Mkoa wa Pwani (RPO), Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Boyd Mwambingu akitolea ufafanuzi moja ya hoja zilizoibuka katika kikao cha Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza Dr. Juma Malewa na wafanyakazi wa vituo hivyo alichofanya mwishoni mwa juma.
Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza Dr. Juma Malewa (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya maafisa na askari wa gereza Wami Kuu na Vijana alipifanya ziara ya kikazi vituoni hapo.
Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza Dr. Juma Malewa (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya maafisa na askari wa Gereza la Mahabusu Morogoro alipofanya ziara mkoani humo mwishoni mwa juma.
Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza Dr. Juma Malewa (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya maafisa na askari wa gereza Kihonda alipofanya ziara ya kikazi kituoni hapo Ijumaa, 27.01.2017.
Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza Dr. Juma Malewa (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya maafisa na askari wa Kingolwira Complex mara baada ya kikao kilicholenga kusikiliza kero na hoja mbalimbali za watumishi hao, tarehe 28.01.2017.
Picha zote na ASP Deodatus Kazinja, PHQ 


Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza Dr. Juma Malewa katika hali ya kuamsha hari na morali ya kufanya kazi kwa watendaji wa Jeshi la Magereza amefanya ziara ya kikazi katika baadhi ya Magereza ya Mkoa wa Morogoro na Pwani mwishoni juma hili.
 
Ziara hiyo imejumuisha Magereza ya Mbigiri, Wami Kuu, Wami Vijna, Mahabusu, Kihonda, Kingolwira Complex yote ya mkoa wa Morogoro na Shule ya Sekondari Bwawani na gereza Ubena vya mkoani Pwani.
 
Kutoka kwa Kaimu Jenerali maafisa na askari aliwapata taarifa fupi ya Uwekezaji wa Ubia katika kiwanda cha sukari cha gereza Mbigiri Mkoani Morogoro kati ya Jeshi la Magereza na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya PPF na NSSF. Alisema uwekezaji huu ni kwa faida ya Jeshi kama Taasisi hivyo ni vizuri kila askari akalifahamu hilo.
 
Katika ziara hiyo pia alipata wasaa wa kufanya vikao na watendaji ambapo maafsa, askari na watumishi raia walipata fursa ya kuuliza maswali moja kwa moja kutoka kwa Mtendaji mkuu wa Jeshi la Magereza ambapo baadhi ya mambo yalipatiwa majibu ya papo hapo na mengine kupewa ahadi ya kutatuliwa katika siku za usoni hasa yenye uhusiano na masuala ya kibajeti.
 
Miongoni mwa masuala yaliyoonekana kuwa ni tatizo sugu ni pamoja na huduma za maji, usafiri, matibabu kwa wafungwa na mahabusu, sare za askari, posho mbalimbali kulingana na stahiki ya kila askari  na mambo mengine madogo madogo ambayo yote kimsingi yanagusia suala la fedha.
 
Katika vikao hivyo Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza Dr. Juma Malewa alitolea maelekezo baadhi ya mambo yaliyohitaji kauli ya Makao Makuu ya Jeshi lakini pia aliwahakikishia kuwa ofisi yake itaendelea kushughulikia kero zote na kusaidia kwa haraka pale inapohitaji kwa kutegemeana na hali ya fedha kwa wakati huo.
 
Kaimu Kamishna Jenerali aliwaasa maafisa askari kuwa waangalifu wanapotumia mitandao ya kijamii hasa kwa kuzingatia viapo vya utumishi wao.
 
“Ninyi ni askari wenye viapo vya utii wa mamlaka zilizopo, jiepusheni na mijadala ya mitandaoni kwani mingine iko kinyume na maadili ya kazi zetu. Ukipokea ujumbe usiofaa futa kabisa badala ya kuusambaza” alisisitiza Dr. Malewa
 
Aidha Dr. Malewa aliwataarifu watumishi hao adhma yake kuu ya kuona Jeshi linakuwa na hospitali kubwa nayakisasa ili kuondoa kero na aibu inayowapata askari na familia zao wanapokuja kutibiwa Jijini Dar es salaam.
 
Ni dhamira yangu kuona tunaanzisha ujenzi wa hospitali hivi karibuni ili kuondoka na adha ambayo wote mnaifahamu, na hospitali hii tutaijenga kwa kutumia vyanzo mbali mbali ikiwemo na sisi kama askari kujitolea. Naomba mtuunge mkono mara wazo hili litakapoletwa kwenu” alisisitiza Kaimu Jenerali.
 
Mwisho aliwataka maafisa na askari kudumisha nidhamu kazini ikiwa ndiyo msingi mkuu wa mafanikio hasa katika kazi za majeshi.