Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini (CGP) Jeremiah Yoram Katungu amewapongeza wakuu wa Magereza mikoa na Magereza yote nchini kwa utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Pongezi hizo amezitoa Aprili 15, 2025 kwenye kikao kazi kilichofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Jeshi la Magereza Msalato jijini Dodoma.
"Ninayo furaha Magereza yote nchini tumeachana na matunizi ya kuni na sasa tunatumia nishati safi ya kupikia" Alisema CGP Katungu.
Pia, CGP. Katungu amewataka kutorudi nyuma katika matumizi ya kuni, badala yake waendelee kutumia nishati safi ya kupikia kama Serikali ilivyoagiza.
Aidha, CGP. Katungu, amewaeleza Wakuu wa Magereza mikoa na Magereza kuwa Jeshi la Magereza limefanya ushirikiano na taasisi ya Elimu na Mafunzo ya ufundi stadi (VETA) na hivi karibuni imeweza kutunuku vyeti wafungwa 201.
Vilevile, Jeshi la Magereza linaendelea na mazungumzo na Chuo cha Uhasibu Arusha ili kuanza kutoa masomo kwa njia ya mtandao(online) kwa kuanzia na masomo ya ujasiliamali kwa wafungwa magerezani.
Pia, CGP Katungu amewataka watumishi wote wa Jeshi la Magereza kudumisha upendo, mshikamano miongoni mwao kwaajili ya maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake,Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, (CP)Nicodemus Tenga
amewataka wakuu hao wa Magereza mikoa na Magereza yote nchini kukusanya taarifa za wafungwa wenye sifa zitakazowezesha kujadiliwa katika Bodi za Parole kwa kuwa mchakato wa kumjadili mfungwa huanzia katika Kamati za urekebishaji ya Gereza, ili wafungwa wenye sifa ya kunufaika na mpango huo wanatakiwa wapatiwe.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Wakuu wa Magereza mikoa na Magereza yote nchini, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mwanza Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Masud Kimolo, alimshukuru Mkuu wa Jeshi la Magereza (CGP) Jeremiah Katungu nakuahidi maelekezo yote ambayo ameyatoa watayatekeleza na kufanya kazi kwa weledi wa hali ya juu kwa manufaa ya Jeshi na Taifa kwa ujumla.