Banner

Banner

Monday, March 17, 2025

KAMATI YA BUNGE MAMBO YA NJE ULINZI NA USALAMA (NUU) YATEMBELEA GEREZA KUU ISANGA.


Kamati ya Bunge Mambo ya Nje Ulinzi na Usalama (NUU) ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Vita Kawawa, Machi 13,2025,  wametembelea Gereza Kuu Isanga jijini Dodoma kujionea miradi mbalimbali inayoendelea katika Gereza hilo pamoja na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Gereza Maalum.


Akizungumza mara baada ya ukaguzi ujenzi wa Gereza Maalum, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Vita Rashid Kawawa ameonesha kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi na kulipongeza Jeshi la Magereza kwa kusimamia kikamilifu Fedha za Serikali katika kutekeleza mradi.


‎Aidha Kamati hiyo imelipongeza Jeshi la Magereza kwa kutekeleza agizo la Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia vema matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiwemo matumizi ya mkaa mbadala(Briquettes),Gas asili(Natural Gas) magerezani na kufanikisha kuondokana na nishati chafu. 

‎Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP) Jeremiah Katungu ameishukuru kamati hiyo kwa mafanikio aliyoyapata kwa bajeti ya mwaka 2023/24 na kufanikisha ukarabati wa Gereza maalum liliopo eneo la Gereza kuu Isanga.

‎"Jeshi linaishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama kwa namna anavyoliwezesha Jeshi la Magereza katika kutekeleza majukumu yake ya msingi ikiwemo miradi ya kimaendeleo" alisema CGP. Jeremiah Katungu.