Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Innocent Lugha Bashungwa (Mb), leo Machi 11, 2025 amezindua Programu ya Urasimishaji wa ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa mafunzo (Recognition of Prior Learning - RPL) na kuwatunuku vyeti vinavyo tambulika na VETA Wafungwa 201 waliohitimu Mafunzo ya fani mbalimbali yaliyotolewa na Jeshi la Magereza.
Akizungumza katika hafla hiyo ya utoaji vyeti Mhe. Bashungwa alisema Programu hiyo itatoa hamasa kwa wafungwa kujifunza na kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za urekebishaji ili kupata ujuzi, elimu, na maarifa kwa ajili ya kuwasaidia kujiajiri au kuajiriwa pindi watakaporudi katika jamii baada ya kutumikia vifungo vyao magerezani.
Kwaupande wake Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP) Jeremiah Yoram Katungu, ameishukuru Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi stadi (VETA) kwa kukubali kuingia makubaliano na Jeshi la Magereza na kutoa vyeti kwa Wafungwa wanohitimu fani mbalimbali Magerezani.
Hafla ya utoaji vyeti kwa Wafungwa ilifanyika Chuo KPF Mkoani Morogoro ambapo Wafungwa waliotunukiwa vyeti wamehitimu katika fani ya Umeme, Ujenzi, ufundi rangi, bomba, magari, upishi, ushonaji na Seremala.