Wednesday, June 3, 2015

Wasifu wa kamishna mkuu mstaafu wa jeshi la Magereza, marehemu Onel Elias Malisa


Marehemu alizaliwa mwaka 1944 katika kijiji cha Kidia, Old Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro.  Alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Kidia mwaka 1951 – 1954 na baadae Shule ya Msingi Kidia Juu (Kidia Upper Primary School) mwaka1955 – 1958.  Alihitimu Elimu ya Sekondari Kidato cha Nne mwaka 1974 katika Shule ya Sekondari Mawenzi akiwa mtahiniwa wa kujitegemea (Private Candate). Aidha, alisoma Cheti cha Sheria Chuo Kikuu cha D’Salaam mwaka 1975 – 1976 na baadaye Shahada ya Kwanza ya Sheria Chuo Kikuu cha D’Salaam mwaka 1977 – 1980. 

Marehemu ajiunga na Jeshi la Magereza mwaka 1964 baada ya kuhitimu Mafunzo ya Awali ya Uaskari Magereza Chuo Ukonga, D’Salaam yaliyofanyika kuanzia Januari - Julai, 1964.  Ndani ya utumishi, alipata fursa ya kuhudhuria Mafunzo ya Uongozi Daraja la Pili (Advance Course) Chuo Ukonga, D’Salaam kuanzia Aprili – Julai, 1967 na Mafunzo ya Uongozi wa Juu (Gazetted Course) kuanzia Februari – Mei, 1974.

Kutokana na utendaji wake wa kazi, marehemu aliwahi kutunukiwa vyeo mbalimbali kama ifuatavyo:-

•    Afisa Magereza Daraja la Tatu mwaka 1964
•    Afisa Magereza Daraja la Pili mwaka 1965
•    Afisa Magereza Mkuu Daraja la Nne mwaka 1967
•    Afisa Magereza Mkuu Daraja la Tatu mwaka 1971
•    Mrakibu Msaidizi wa Magereza mwaka 1975
•    Mrakibu wa Magereza mwaka 1976
•    Mrakibu Mwandamizi wa Magereza mwaka 1978
•    Kamishna Msaidizi wa Magereza mwaka 1982
•    Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza mwaka 1984
•    Kamishna wa Magereza mwaka 1992
•    Kamishna Mkuu wa Magereza mwaka 1996 – 2002

Aliwahi kufanya kazi katika vituo mbalimbali vikiwemo Gereza Butimba -  Mwanza, Isanga - Dodoma, Wami Vijana - Morogoro, Chuo cha Usalama Moshi,  Gereza Songwe - Mbeya, Chuo Ukonga - D’Salaam na Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, D’Salaam.

Aidha, marehemu aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya Jeshi la Magereza kama ifuatavyo:-

•    Mkufunzi Mkuu Chuo Ukonga mwaka 1975
•    Mkuu wa Chuo Msaidizi, Chuo Ukonga mwaka 1981
•    Mkurugenzi Msaidizi wa Sheria na Urekebishaji, Makao Makuu mwaka 1983
•    Mkurugenzi wa Sheria na Urekebishaji, Makao Makuu mwaka 1984
•    Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, Makao Makuu mwaka 1992
•    Kamishna Mkuu wa Jeshi la Magereza mwaka 1996 – 2002 alipostaafu kazi.


Marehemu atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa alioutoa wakati wa utumishi wake.  Baadhi ya mambo aliyoyafanya ni kama ifuatavyo:- 

•    Alianzisha na kuimarisha mahusiano baina ya Jeshi la Magereza na Magereza ya nchi nyingine Afrika na duniani. 
•    Alikuwa mmojawapo wa Makamishna wa Tume ya Marekebisho ya Sheria Nchini (Law Reform Commission)
•    Alikuwa mshauri kwenye Maboresho ya Jeshi la Magereza pamoja na Sera ya Taifa ya Magereza.
•    Kama hatua ya kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani aliweza kushauri  na kusimamia kutungwa kwa Sheria zifuatazo:-

-    Sheria ya Bodi ya Parole
-    Sheria ya Huduma kwa Jamii (Community Service)

Nishani alizotunukiwa akiwa kazini ni:-

•    Nishani ya mstari wa nyuma
•    Nishani ya Utumishi mrefu
•    Nishani ya Utumishi uliotukuka

Hata baada ya kustaafu kazi, marehemu aliendelea kutoa mchango wake kwa kushauri mambo kadhaa pamoja na kushiriki kwenye matukio mbalimbali ya Jeshi na Taifa.  Kutokana na mchango wake huo alitunukiwa Nishani ya Kumbukumbu ya Miaka 50 ya Muungano Daraja la Nne na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 26 Aprili, 2015.
Kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa Magereza na Watumishi wote wa Jeshi la Magereza, tunatoa salamu nyingi za rambirambi kwa Mke, Watoto na Ndugu wa Marehemu kwa msiba huo mkubwa uliotufika.

MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU MAHALI PEMA PEPONI, AMINA